About Company
WASIFU WA HALMASHAURI
1.0 Utangulizi
Wilaya ya Kakonko ilianzishwa kwa tangazo la Serikali GN. 287 ya mwaka 2011 baada ya kugawa Wilaya ya Kibondo na kuunda Wilaya ya Kibondo na Kakonko. Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ilianzishwa tarehe 08/3/2013 na kutangazwa katika gazeti la Serikali kwa GN.42. Aidha ilizinduliwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali (Mst) Issa Saleh Machibya tarehe 19 Agosti, 2013 katika ukumbi wa Jumba la Maendeleo Kibondo.
Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya yapo katika mji wa Kakonko uliopo umbali wa Km 48 Kaskazini mwa mji wa Kibondo katika barabara kuu ya Kigoma – Mwanza.
1.1 Jiografia ya Mahali ilipo Wilaya
Wilaya ya Kakonko ni mojawapo ya Wilaya 6 za Mkoa wa Kigoma. Wilaya ipo upande wa kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na inapakana na Wilaya ya Ngara na Biharamulo (Mkoa wa Kagera) kwa upande wa Kaskazini na Magharibi inapakana na Jamhuri ya Burundi, Kusini inapakana na Wilaya ya Kibondo, Mashariki hadi Kaskazini Mashariki inapakana na Wilaya ya Bukombe (Mkoa wa Geita).
1.2 Ukubwa wa Wilaya
Wilaya ya Kakonko ina ukubwa wa kilometa za mraba 7,715.05 na eneo lililopo ndani ya mamlaka ya vijiji ni Km za mraba 2,041.03 sawa na 26.5% na eneo la msitu wa hifadhi ni Km za mraba 178.65 sawa na 2.3%. Wilaya ina km za mraba 1,084.2 za ardhi inayofaa kwa kilimo sawa na 14.1%, hata hivyo ardhi inayolimwa ni km za mraba 671.8 sawa na 62% ya ardhi inayofaa kwa kilimo, Aidha Wilaya ina kilometa za mraba 806.4 ya ardhi ya malisho sawa na 10.5%.
Hifadhi ya akiba ya wanyamapori ya Moyowosi (Moyowosi Game Reserve) na Msitu wa Hifadhi ya Wilaya (Buyungu Local Authority Forest Reserve) una ukubwa wa kilometa za mraba 624.9 sawa na asilimia 8.1 na Maeneo yanayobaki ni ya makazi, huduma za jamii, milima na maji.
1.3 Idadi ya Watu na Shughuli za Kiuchumi
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Wilaya ilikuwa ina jumla ya watu 167,555; Wanaume 81,417 na wanawake 86,138. Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kufikia mwaka 2021 Wilaya ya Kakonko inakadiriwa kuwa na Watu 230,955 ikiwa ni Wanaume 113,504 na wanawake 117,451 ikiwa ni wastani wa 2.4% ya ongezeko la watu kwa mwaka na jumla ya kaya 51,933 ambapo kaya 43,105 (82.6%) hujishughulisha na kilimo na kaya 8,828 (17.4%) ni wafugaji wa wanyama, nyuki na samaki, biashara ndogo ndogo, ufundi na utunzaji wa mazingira.
1.4: Hali ya Hewa
Hali ya hewa ni nyuzi joto kati ya 150C hadi 220C na hupata mvua kati ya 800mm hadi 1,900mm kwa mwaka kuanzia Oktoba hadi mwisho wa Mei.
2.0 Sekta ya Utawala
Wilaya ya Kakonko ina jumla ya Tarafa tatu (3) ambazo ni Nyaronga, Kasanda na Kakonko ambazo zina jumla ya Kata kumi na tatu (13), vijiji 44 na Vitongoji 355.
Utawala bora na uwajibikaji ni mojawapo ya maeneo muhimu yanayopewa kipaumbele na Serikali kupitia Ilani ya uchaugzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, Dira ya maendeleo ya Taifa 2025, Mkakati wa Maendeleo Endelevu (SDG) na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/2022 – 2025/2026).
Kero na malalamiko mbalimbali ya wananchi hutatuliwa kupitia Ofisi za Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji, Waheshimiwa Madiwani na Watendaji wa Kata, Mkurugenzi Mtendaji, Ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Aidha Halmashauri ina dawati maalumu linaloshughulikia malalamiko mbalimbali yanayoletwa dhidi ya Halmashauri au Watendaji wake na kufanya ufuatiliaji kuhakikisha kila lalamiko la mwananchi linatatuliwa au kuelekezwa kwenye mamlaka inayohusika. Baadhi ya malalamiko ama kero ni kama Migogoro ya Ardhi, Migogoro ya unyanyasaji wa Kijinsia na mingine. Kero nyingi hutatuliwa kupitia dawati la malalamiko kwa kuwasiliana ama kushirikiana na wahusika wa maeneo au idara husika. Pia masanduku ya maoni yamewekwa katika Ofisi ili kubaini kero mbalimbali na kuzipatia ufumbuzi mapema.